Tanzania, lulu ya Afrika Mashariki, inazidi kung’aa kama moja ya vivutio bora zaidi vya utalii barani Afrika. Ikiwa na mandhari ya kuvutia, urithi tajiri wa kitamaduni, na sifa inayokua ya amani na ukarimu, nchi yetu imeandikisha ongezeko la ajabu la watalii kutoka 1,711,625 mwaka 2021 hadi 5,360,247 mwaka 2024. Huu ni msingi imara wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii cha bara zima.

Nchi yetu imebarikiwa na baadhi ya vivutio maarufu zaidi duniani. Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko yote barani Afrika, unaendelea kuwavutia wapandaji na wapenda matukio kutoka pande zote za dunia. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, maarufu kwa uhamaji mkubwa wa nyumbu na pundamilia, bado ni mojawapo ya matukio ya ajabu zaidi ya wanyama duniani. Bonde la Ngorongoro linatoa makazi ya kipekee yaliyojaa wanyama na linachukuliwa kuwa moja ya mifumo ya ikolojia yenye wingi mkubwa wa viumbe barani Afrika.

Zaidi ya wanyamapori, Tanzania inatoa uzoefu mbalimbali ambao ni nadra kupatikana sehemu nyingine. Visiwa vya Zanzibar, vilivyopambwa na harufu ya viungo na historia ndefu ya mchanganyiko wa utamaduni wa Kiswahili, Kiarabu na Ulaya, vinatoa mwanga wa kuvutia wa urithi wa karne nyingi. Fuko safi za bahari za Pemba na Mafia zinawakaribisha wageni kwa mapumziko, kupiga mbizi, na kuchunguza miamba ya matumbawe yenye uhai mwingi. Mbuga za kusini kama Ruaha,Katavi na Nyerere zinapata umaarufu kwa mandhari yake ya pori lisiloguswa na utulivu wa kipekee.

Nguvu kubwa ya Tanzania iko katika amani na utulivu wake. Wakati baadhi ya maeneo duniani yanakabiliwa na changamoto za kiusalama, Tanzania imeendelea kudumisha rekodi ya kipekee ya amani, na kuifanya kuwa mahali salama na pa kuvutia kwa watalii. Mazingira haya ya utulivu yanavutia wawekezaji wa muda mrefu na kuongeza ubora wa uzoefu wa wageni.

Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo viwanja vya ndege, barabara, na huduma za kidijitali hivyo kufanya safari ndani ya nchi kuwa rahisi na salama zaidi. Kampeni kama filamu ya “The Royal Tour” zimeisaidia Tanzania kung’aa zaidi kimataifa.

Hii ni fursa ya dhahabu kwa vijana, wafanyabiashara na familia kushiriki katika sekta ya utalii. Kuanzia kuanzisha hoteli ndogo, lodges, migahawa, biashara ya ufundi, huduma za usafiri, kuongoza watalii, hadi kutoa mazao ya asili na vyakula vya kienyeji,fursa zipo nyingi na zinazidi kukua kila mwaka.

Muongoza Watalii Daniel Moshi kutoka Arusha anasema, “Nimefanya kazi ya kuwa tour guide kwa miaka mingi. Watalii wanaongezeka sana na wengi wanasema Tanzania ni salama na ya kipekee. Vijana wetu wasikose fursa hii. Wawekeze katika utalii kwa kuanzisha kampuni ndogo ya usafiri au kutoa huduma za watalii kunaweza kuwaletea maisha mazuri.”

Naye Dereva wa Magari ya Watalii Bi Fatuma Hassan kutoka Moshi anasema, “Kila siku ninaendesha watalii kwenda Kilimanjaro na Serengeti. Mapato yangu yameongezeka sana tangu 2021. Amani yetu inavutia wageni wengi. Ninawahimiza vijana na wafanyabiashara wa Arusha na Kilimanjaro kushiriki kwa kuanzisha biashara zinazohusiana na utalii. Fursa ipo sasa.”

Pia Mwandishi aliongea na Bwana Elias Kileo ambaye n mbeba mizigo ya watalii kutoka Marangu, Kilimanjaro, anahitimisha, “Kilimanjaro imenipa riziki kwa miaka mingi. Wapandaji wanaongezeka na wengi wanarudi tena kwa sababu ya amani na ukarimu wa watu wetu. Vijana tuchukue hatua sasa , tujifunze ustadi wa utalii, tuwekeze katika lodges au huduma za wapandaji. Utalii unaweza kutuletea maendeleo ya kweli.”

Kwa vivutio vyake vya asili, usalama, na watu wenye tabasamu, Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kuwa nchi bora kabisa ya utalii barani Afrika. Huu ni wakati wa Watanzania kuchukua hatua ya kuchunguza, kuwekeza, na kushiriki katika sekta ya utalii ili kujenga mustakabali wetu na wa vizazi vijavyo.